Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kukabiliana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia na kuondoa madhara ya kiafya, ni wakati wa jamii kubadili fikra na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia kwani kwa sasa matumizi ya gesi sio anasa.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambapo amezitaka taasisi zote za serikali na binafsi zinazohusika na mkakati mzima wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza mkakati huo kwa kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana nchi nzima na kwa bei nafuu.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni mahitaji ya lazima sasa na sio anasa [..] Gesi haina hatari inategemea unavyoitumia. Wizara na taasisi na mashirika yasiyo ya serikali yapo tayari kutoa mafunzo mpaka vijijini kuhusu matumizi ya gesi kwa kupikia,” amesema.
Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati kubuni mpango wa kuwawezesha watumiaji wa gesi ya kupikia kulipia kadri wanavyotumia kama inavyofanyika kwenye LUKU za umeme.
“Sekta binafsi tunaitarajia pamoja na kuongeza uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia sehemu mbalimbali nchini, watuletee pia teknolojia rahisi itakayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyika kwa umeme na maji,” ameeleza.