Baadhi ya shughuli zakwamishwa na kukosekana kwa mtandao Afrika Mashariki
Nchi kadhaa za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania zimekumbwa na kuzorota kwa huduma za mtandao baada ya kubainika kuwa ni kutokana na hitilafu katika nyaya za chini ya bahari.
Kwa mujibu wa Cloudflare Radar, ambayo hufuatilia uunganishaji wa Intaneti, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na trafiki kushuka hadi asilimia 30 ya viwango vinavyotarajiwa.
Kukatika kwa mtandao nchini kumekuwa na athari kubwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo za afya, benki na vyombo vya habari. Pia katika baadhi ya hospitali, utoaji wa huduma umekuwa ukikwama huku wagonjwa wakipata ucheleweshaji wa kupata matokeo ya matibabu.
Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye amesema wakati utatuzi wa tatizo hilo ukiendelea, upatikanaji wa huduma za intaneti pamoja na huduma za simu za kimataifa utakuwa wa kiwango cha chini kwa kutumia njia mbadala mpaka tatizo husika litakapotatuliwa.
Afisa mkuu wa kikundi cha teknolojia na uvumbuzi wa Liquid Intelligent Technologies, Ben Roberts ameeleza kuwa taarifa walizonazo zimethibitisha kwamba moja ya nyaya za chini ya bahari inaonekana kukatwa kilomita 45 kaskazini mwa Durban, Afrika Kusini hivyo kusababisha mtandao kuwa chini.
Baadhi ya kampuni za mawasiliano zimekiri changamoto hiyo, ikiwa ni pamoja na Safaricom ya Kenya, ambayo imesema inakabiliwa na changamoto huku Cloudflare Radar pia ikiripoti kuwa Malawi, Msumbiji, na Madagascar zimeathirika.
Mnamo Machi, mwaka huu sehemu za Magharibi na Kusini mwa Afrika pia zilikabiliwa na shida kama hiyo ambayo iliathiri nchi zikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Ivory Coast, Liberia, Benin, Ghana na Burkina Faso.
Kukatika kwa mtandao kwa wingi kulitokana na uharibifu unaotokana na nyaya za baharini za MainOne na ACE. Mfumo wa Cable wa SAT-3/West Africa (WACS), Pwani ya Afrika hadi Ulaya (ACE), MainOne, na Atlantiki ya Kusini 3 zote ziliathiriwa mwezi Machi.