Watu 11 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mfumo wa joto wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mtibwa kulipuka wakati wakijiandaa kuanza uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho kilichopo Turiani mkoani Morogoro.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo amesema mlipuko huo ulitokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa saba usiku na umesababisha vifo vya watu 11 na wengine wawili kujeruhiwa.
“Ni kweli watu 11 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mlipuko wa mpira wa joto wakati wanajiandaa na uzalishaji wa sukari pale kiwandani.
Ifahamike ili sukari ichakatwe kuna kiwango cha joto ambacho kinatakiwa kifikie, sasa wakati maandalizi ya uzalishaji yakifanyika na kile kiwango cha joto kikingojewa ndipo ukatokea mlipuko huo na kuwakuta watu hao 11 ambao kwa kiwango kile cha joto wakafariki papo hapo,” amesema Marugujo.
Aidha, amesema chanzo cha mlipuko huo bado hakijajulikana na jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na taarifa rasmio itatolewa baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Chanzo: Mwananchi