Watanzania waishio Vatcan wamwombea Rais Samia na taifa
Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki waishio Vatican wamefanya ibada maalum ya kufunga mwaka wa masomo pamoja na kutumia ibada hiyo kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi wengine wa Tanzania pamoja na taifa kwa ujumla.
Jumuiya hiyo inaundwa na watumishi wa Mungu takribani 302 wakiwemo mapadre, mashemasi, watawa na mafrateri ambao wanapata elimu katika vyuo vikuu vya Vatican na wanatoa huduma za kiroho sehemu mbalimbali eneo hilo na Italia.
Ibada hiyo iliambatana na hafla ya kuwaaga wale waliohitimu mafunzo yao na kuwakaribisha wanafunzi wapya kutoka Tanzania ambapo Balozi wa Tanzania-Vatican, Hassan Mwamweta ambaye ni mlezi wa Jumuiya hiyo alishiriki pamoja na Balozi Mahmoud Kombo anayeiwakilisha Tanzania nchini Italia.
Mwezi Februari mwaka huu Rais Samia akiwa kwenye ziara ya kikazi Vatican, alikutana na wanajumuiya hiyo pamoja na diaspora wengine ambapo pamoja na mambo mengine alifanya mazungumzo nao na kushiriki pamoja hafla ya chakula cha jioni.