Tanzania yashinda shindano la TEHAMA China
Vijana watatu wa Kitanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika Ndaki ya ICT (CoICT) wameibuka washindi katika mashindano ya TEHAMA duniani upande wa Tuzo Kuu za Mashindano ya Mazoezi na Ubunifu ya Huawei yaliyofanyika Mei 23 hadi 26, mwaka huu Shenzhen, China.
Vijana hao ambao ni Dickson Mram, Matimu Mahimbo na James Amos wenye ujuzi katika uhandisi wa kompyuta, IT na mawasiliano ya simu, waliambatana na Mhadhiri msaidizi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Jumanne Ally na kushiriki katika mashindano hayo yaliyowashindanisha wanafunzi zaidi ya 470 kutoka nchi 49 duniani.
Akizungumzia kuhusu ushindi huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema ushindi huo unaonyesha uwezo uliopo miongoni mwa vijana wa Kitanzania katika fani muhimu za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Ameongeza kuwa washindi hao ambao watarejea nchini Mei 28, 2024 watapokelewa kwa shangwe na kupongezwa kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengine wa kitanzania.