Mkurugenzi wa Tume ya UKIMWI Zanzibar, Dkt. Ahmed Mohamed Khatib amesema ingawa idadi ya watu wanaopata maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi inapungua nchini, lakini kuna changamoto kwa vijana wa kike wenye umri kati ya miaka 15-24 kupata maambukizi Zanzibar, ambapo idadi hiyo inazidi kuongezeka.
Akizungumza na wadau wa kupambana na maambukizi ya VVU Zanzibar, amesema miongoni mwa vitu vinavyochangia maambukizi makubwa kwa kundi hilo la wanawake vijana ni udhalilishaji wa kijinsia ambapo utafiti umeonesha vijana wa kike watatu kati ya 10 wanadhalilishwa.
Aidha, amesema tatizo la UKIMWI Zanzibar lipo zaidi katika makundi maalum matatu wakiwemo wanawake wanaofanya biashara ya kuuza mwili, wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano.
Amebainisha kuwa katika utafiti uliofanywa mwaka 2007, wanawake wanaouza miili yao wana asilimia 21.1 ya maambukizi ya VVU, wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ni asilimia 11.4 na vijana wanaotumia dawa za kulevya ni asilimia 9.3.
Chanzo: Nipashe