Nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe hataruhusiwa kuvaa barakoa yenye rangi tatu inayofanana na bendera ya taifa ya Ufaransa atakaporejea kucheza katika Mashindano ya UEFA Ulaya nchini Ujerumani siku ya Ijumaa dhidi ya Uholanzi.
Mbape alionekana akiwa amevalia barokoa yenye rangi nyeupe, nyekundu, na bluu za bendera ya taifa ya Ufaransa wakati wa mazoezi mepesi na wachezaji wenzake siku ya Alhamis.
Kwa mujibu wa kanuni za UEFA, mchezaji ataruhusiwa kuvaa barakoa ya rangi moja pekee wakati wa mechi, isipokuwa kama kuna msamaha maalum.
“Vifaa vya matibabu vinavyovaliwa kwenye uwanja wa mchezo lazima viwe na rangi moja na visiwe na alama za timu au mtengenezaji,” inasomeka sehemu ya kanuni za UEFA.
Nahodha huyo alivunjika pua baada ya kugongana na beki wa timu pinzani, Kevin Danso wakati wa mechi dhidi ya Austria siku ya Jumatatu na kulazimika kutoka nje ya uwanja huku kukiwa na wasiwasi endapo ataweza kumaliza mechi zilizobaki za hatua ya makundi.
Uamuzi bado haujafanywa kama ataweza kucheza dhidi ya Uholanzi siku ya Ijumaa, ingawa meneja Didier Deschamps alithibitisha katika mkutano wa waandishi wa habari kabla ya mechi kwamba mshambuliaji huyo anaendelea vizuri zaidi.