Kesi ya Kabendera akiituhumu Vodacom kufanikisha kutekwa kwake kusikilizwa leo
Kesi ya mwanahabari, Erick Kabendera aliyoifungua dhidi ya kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom inasikilizwa leo katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Mfawidhi, Salaam Maghimbi.
Katika kesi hiyo, Kabendera ambaye alikuwa amejikita katika uandishi wa Habari za uchunguzi, anadai kampuni ya Vodacom imlipe fidia ya Dola za Marekani milioni 10 [TZS bilioni 26.5] akiituhumu kuwa ilifanikisha tukio aliloliita kutekwa na askari Polisi, na kisha kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi mwaka 2019.
Kabendera amedai kutokana na matukio hayo ameathirika kiuchumi, kijamii, kisaikolojia, kutoaminiwa kitaaluma na masuala mengine binafsi pamoja na kutaka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadiri mahakama itakavyotathmini.
Aidha, katika hati ya wito wa mahakama iliyotolewa na mahakama kwa pande zote mbili, imeitaka kampuni ya Vodacom kufika mahakamani bila kukosa ikiwa na nyaraka zote ambazo itazitumia katika kesi hiyo.