Baada ya Simba SC kushusha mastaa kutoka sehemu mbalimbali akiwemo mchezaji ambaye alikuwa wa kwanza kutambulishwa klabuni hapo, beki wa Coastal Union, Lameck Lawi ameeleza kuwa yeye ni mchezaji halali wa Coastal Union.
Inaelezwa kuwa usajili huo ambao ulikuwa mkataba wa miaka mitatu kwa gharama ya shilingi milioni 230 umegonga mwamba kutokana na kukiukwa kwa taratibu za usajili na pande zote mbili kushindwa kuelewana.
“Nipo Dar es Salaam na Coastal Union kwa sababu ni mchezaji wa hii timu, tumekuja hapa kwa ajili ya kambi tunajiandaa na michuano ya Kagame,” ameeleza Lawi katika mahojiano na Mwanaspoti.
Akizungumza Afisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally amekiri kuwa ishu ya Lawi ina utata, hivyo suala hilo litatolewa ufafanuzi hapo baadaye.
Simba SC iko nchini Misri kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.