Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amemwagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda kuwafukuza kazi watumishi wa mamlaka hiyo wanaoomba na kupokea rushwa kwani vitendo hivyo vinaitia doa serikali na kuikosesha mapato.
Akizungumza katika kikao cha Tathmini ya Utendaji Kazi TRA kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Dkt. Nchemba amesema mbali na kuwafukuza kazi watumishi hao, mamlaka iwachukulie hatua kali za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani ili iwe funzo kwa wengine.
Aidha, amemwagiza kamishna huyo kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara wasiowasilisha ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa kuwa fedha hizo zinatakiwa kuwasilishwa serikalini kupitia TRA.
Pamoja na hayo, amewataka watumishi wa TRA kuongeza ubunifu, umahiri na kuhakikisha wanatenda haki wakati wa kukusanya mapato ya Serikali ili kutimiza matarajio ya Rais Samia Suluhu ya kuwaletea watanzania maendeleo ya uhakika.