Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wahasibu Afrika

0
43

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG)) utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia Desemba 03 hadi 05, mwaka 2024 ukiwahusisha zaidi wa washiriki 2,000 kutoka takriban nchi 55 za Bara la Afrika.

Akizungumza Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude wakati wa mkutano na waandishi wa Habari jijini Arusha, amesema mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, hususan kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.

Amesema faida nyingine za mkutano huo ni pamoja na kuwa na Afrika yenye mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, Bara jumuishi lililounganishwa kisiasa kwa kuzingatia maadili ya Pan-Africanism.

Amesema manufaa mengine ni pamoja na kuwa na maono ya mwamko wa Afrika na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, Afrika yenye amani na usalama na Afrika yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.

CPA Mkude amesema mkutano huo utawaleta wahasibu wakuu wa Serikali Afrika watakaoambatana na Wahasibu Wakuu wa Wizara, Taasisi za umma na Wahasibu na wadau wengine ambao watapata fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma na kubadilishana mawazo na kujua fursa zinazopatikana katika nchi za Afrika.

Send this to a friend