Waziri Ndejembi aagiza hati za ardhi zitolewe kwa wakati
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amewataka Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Ardhi kuondoa urasimu na kutoa hati milki za ardhi kwa wakati.
Ameyasema hayo leo wakati wa kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo mara baada ya kupokelewa Makao Makuu ya Wizara yaliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
“Tuondoe urasimu, kama mtu ana nyaraka zote zinazohitajika, tuwape hati zao na tukumbuke sisi ni watoa huduma kwa wananchi na ni wizara wezeshi, hati zitolewe kwa wakati na hati zilizo tayari wananchi wajulishwe waje wachukue hati zao” amesema.
Ameongeza kuwa, “Sijaja kutengua kazi mnazoendelea kuzifanya, nimekuja kuongeza nguvu. Tuzidi kufanya kazi vizuri na kuhakikisha mifumo yetu ya kiwizara kuanzia wilaya, mikoa na wizara ifanye kazi vizuri. Ni vizuri tusimamie haki ya wananchi na mifumo ifanye kazi yake kutoa haki.”
Aidha, Ndejembi amesisitiza kuendelea kwa Klinik za Ardhi ambapo amesema kasi katika kliniki hizo lazima iongezwe kwa kuwa wakati mwingine wananchi inakuwa vigumu kuwafikia makamisha wa ardhi wasaidizi wa mikoa.