Rais Samia aagiza utafiti wa kitaifa kuhusu wataalam wa afya kwenye soko la ajira

0
110

Rais Samia ameiagiza Wizara ya Afya kukamilisha utafiti wa kitaifa kubainisha hali halisi ya wataalam wa afya nchini walioko kwenye soko la ajira ili serikali itambue nguvu kazi iliyoko nje ya vituo vya tiba ikiwemo kwenye soko la ajira.

Akizungumza wakati wa kilele cha Kumbukukizi ya 3 ya Urithi wa Benjamin Mkapa, Rais Samia amesema Serikali inampango wa kuajiri wahudumu wa afya 137,000 kwa kipindi cha miaka kadhaa pamoja na kuendelea kushughulikia maslahi ya watumishi wa afya moja baada ya jingine.

“Serikali pia ina mpango wa kuajiri wahudumu [wa afya] 137,000 kwa kipindi cha miaka kadhaa na nimetaarifiwa kwamba tayari mchakato wa kuwapata umekamilika katika ngazi ya Halmashauri na mafunzo ya kundi la awamu ya kwanza yataanza mwezi huu katika vyuo vya afya nchini,” amesema.

Aidha, amesema Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa ni Baba wa taasisi, mifumo na mageuzi kutokana na vitu alivyovianzisha katika sekta mbalimbali hapa nchini ambavyo vinatumika hadi sasa.

“Urithi aliotuachia Hayati Rais Benjamin Mkapa, unamfanya aendelee kuishi hata baada ya kifo chake. Mzee Mkapa anakumbukwa kama Baba wa taasisi, Baba wa mifumo na Baba wa mageuzi, yaani alikuwa amejishughulisha sana kwenye kuanzisha taasisi, mifumo na mageuzi.

Aliamini sana katika mambo hayo matatu katika kipindi cha Urais wake, alitumia muda mwingi wa hotuba zake kuelezea umuhimu wa mageuzi, mifumo na ujenzi wa taasisi katika sekta zote,” ameeleza.

Mbali na hayo, ameipongeza taasisi ya Benjamin Mkapa kwa mchango wake katika sekta ya afya akieleza kuwa ndani ya miaka 18 taasisi hiyo imesomesha watumishi wa afya watarajiwa na watumishi walioko kazini takribani 1100 katika fani mbalimbali zikiwemo za matibabu, wauguzi wakunga nakadhalika.

Send this to a friend