Tanzania kinara Afrika Mashariki kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii

0
30

Ripoti ya Mapitio ya Hali ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2024 iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii na kuwa kinara miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, licha ya changamoto zinazoikabili dunia ikiwemo athari za UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na mizozo ya vita inayoendelea maeneo mbalimbali duniani.

Riooti hiyo imezinduliwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) kwa njia ya mtandao akiwa Abuja nchini Nigeria, ambako anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings), wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Aidha, ripoti hiyo ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na unatarajia kupanda kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023, hadi asilimia 5.7 mwaka 2024, na utafikia asilimia 6 mwaka 2025.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uchumi wake kupitia Mpango wake wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III), wenye lengo la kujenga uchumi imara, shirikishi na wenye ushindani kupitia sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, uzalishaji viwandani, kuongeza thamani ya bidhaa, uwekezaji na biashara pamoja na kukuza ajira kwa wananchi hususan vijana.

Mbali na hilo, amezitaka Taasisi za Fedha za Kimataifa, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuweka mazingira ya upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu ili kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na uwezo endelevu wa kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ajili ya nchi zao.

Dkt. Nchemba ametaja eneo linalokwamisha maendeleo ya nchi hizo za Kiafrika ikiwemo Tanzania kuwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo kila mwaka Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 6.3 za kukabiliana na hali hiyo zikiwemo athari za papo kwa papo zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

 

 

 

 

 

 

 

Send this to a friend