Ofisi ya Msajili wa Hazina, PSSSF na WCF zaingia ubia kumiliki kiwanda cha chai Mponde
Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), wameingia ubia wa kumiliki Kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo mkoani Tanga kwaajili ya kuongeza tija katika uzalishaji, huku wadau mbalimbali wakitakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika zao la chai.
Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya kumiliki kiwanda hicho, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema uwekezaji huo unakwenda kuongezeka thamani ya kiwanda kutoka shilingi milioni 790 zilizopo na kufikia bilioni 4.8.
“Kiwanda hiki kinakwenda kufufua uchumi kwa wakazi wa Korogwe na wakulima wa zao la chai watapata fursa ya kupata soko la uhakika wa kuuza mazao yao” amesema.
Mchechu ameongeza kuwa kupitia uwekezaji huo, Serikali inakwenda kunufaika na ulipaji wa kodi, huku akisisitiza umuhimu wa Menejimenti kuongeza ufanisi katika utendaji ili waweze kuleta gawio kama ilivyo kwa taasisi nyengine.
Katika ubia huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba Serikali inamiliki hisa ya asilimia 16, huku PSSSF na WCF wakimiliki asilimia 42 kila mmoja.