Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Jeshi la Polisi kuwaachilia huru bila masharti yoyote viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadhi ya waandishi wa Habari ili waweze kutekeleza wajibu na haki za kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesema LHRC inalaani hatua ya Jeshi la Polisi kuwashikilia baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA baada ya kupanga kufanya kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwenye uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.
Aidha, amesema kwa mujibu wa ibara ya 20 ya Katiba ya Tanzania yam waka 1977, kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa sura Na.258 na marekebisho yake ya mwaka 2024, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981, ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, makongamano pamoja na maandamano.
Mbali na hivyo, LHRC imesema inaendelea kufuatilia tukio hilo kwa karibu na kwa hatua zaidi.
Agosti 11, 2024, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko iliyopangwa na viongozi wa chama hicho kwa mwamvuli wa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kutokana na kauli walizozitoa ambazo zimetafsiriwa kuwa zinahatarisha amani.