Mtoto wa miaka minne alenga na kuvunja dirisha la basi la Shabiby kwa manati

0
27

Safari ya abiria wa basi la Shabiby Line kutoka Mbeya kuelekea Dodoma ilikumbwa na kadhia isiyotarajiwa hapo jana, baada ya mvulana mwenye umri wa miaka minne kutoka kijiji cha Ndolela, Iringa, kuvunja kioo cha basi hilo kwa kutumia manati akiwa upande wa pili wa barabara.

Tukio hilo lilisababisha kucheleweshwa kwa safari kwa takriban saa moja na nusu, huku abiria wakishuka kwa hasira kumtafuta mvulana huyo, ambaye alikimbilia nyumbani kwa bibi yake kujificha mara baada ya kufanya tukio hilo na kufanikiwa kukamatwa.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo tayari amewahi kusababisha tukio kama hilo hapo awali, ambapo bibi yake alilazimika kulipa Shilingi 170,000 kufidia uharibifu wa kioo cha basi.

Basi hilo, ambalo lilitarajiwa kuwasili Dodoma saa 8:30 mchana, hatimaye lilifika saa 10:15 jioni, likiwa limechelewa kwa zaidi ya saa moja na nusu. Ingawa hakuna abiria aliyejeruhiwa, japokuwa mmoja wa abiria alinusurika kugongwa na jiwe lililorushwa.

Wasiwasi umeongezeka kuhusu tabia ya hatari ya mvulana huyo, ambayo inaweza kusababisha ajali kubwa na hatari zaidi katika siku zijazo. Wazazi na wakazi wa kijiji hicho wamehimizwa kumchunga mtoto huyo kwa karibu ili kuepuka matatizo kama hayo kuendelea kutokea.

Send this to a friend