Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imewahukumu Elikana Pamasi (19) na Saguda Hushi (42) wote wakazi wa Kijiji cha Kayenze Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili.
Washtakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 9, 2020 katika Kijiji cha Kapanga ambapo walimuua kwa makusudi Juma Cherehani (26) kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumnyang’anya pesa Shilingi milioni 1.8 ambapo Jeshi la Polisi liliwakamata Machi 18, 2020 na kufikishwa mahakamani Machi 26, 2020.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 15, 2024 chini ya Jaji Mwenempazi TM baada ya kuridhishwa na ushahidi wa bila mashaka uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Mwenempazi amesema washtakiwa hao wametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na kueleza adhabu hiyo imetolewa ili iwe fundisho kwa washtakiwa na jamii katika kukomesha vitendo vya kikatili.