Familia ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (SSP), Fatuma Kigondo imesema inafikiria kufungua mashtaka dhidi ya wote waliosambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa ndugu yao amehusika kutuma vijana kufanya ukatili kwa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Akiandika katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Emmanuel Muga amesema familia hiyo inataka kuhakikisha haki inatendeka na ukweli wa jambo hilo unawekwa wazi.
Amesema familia hiyo imeeleza kuwa SSP Fatuma siyo afande anayezungumziwa kwenye video hiyo na kwamba ndugu yao ni Ofisa wa Polisi mwenye cheo cha SSP na si ASP kama inavyoelezwa katika mitandao ya kijamii.
“Familia imethibitisha kuwa SSP Fatuma ni mjane na hana mume ambaye angeweza kuporwa kama ilivosemwa,” ameeleza.
Aidha, amesema famili hiyo imefafanua kuwa washukiwa wa ubakaji wamebainika kuwa wanatoka kwenye vikosi vingine visivyo chini ya amri ya SSP Fatuma, hivyo inawapa maswali kuwa ofisa huyo angewezaje kutoa maagizo kwa washukiwa hao, iwe ni kisheria au isivyo kisheria.
Chanzo: Nipashe