Washiriki zaidi ya 500 kushiriki Wiki ya AZAKI 2024
Washiriki zaidi ya 500 kutoka Asasi za Kiraia (AZAKI), Sekta Binafsi, Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024, itakayofanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13 Jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, amesema wiki hiyo imebebwa na kauli mbiu ya Sauti, Dira na Thamani, ikiendana na wakati uliopo na matukio yanayoendelea nchini, ambayo ni pamoja na uchaguzi wa Serikali za mtaa utakaofanyika mwaka huu, uchaguzi mkuu wa mwakani na Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Mwakani tunatarajia kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo ni fursa adimu sana inayokuja mara moja kwa muda mrefu. Fursa hii kutokana na umuhimu wake si budi sauti za wananchi zikasika kuchangia maoni yao wenye, kwani dira ya Taifa inapaswa itokane na sauti, mawazo, mitazamo na maoni ya wananchi,” amesema Rutenge.
Ameongeza kuwa, wiki hiyo pia itakuwa na mijadala mbalimbali inayohusu shughuli za AZAKi nchini, maendeleo ya jamii na ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia, Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika kusaidia na kuwezesha watu wenye ulemavu wa macho nchini (CBM), Nesia Mahenge ameeleza kuwa, katika wiki hiyo itayaleta pamoja makundi mbalimbali ikiwemo vijana, jamii, makundi maalum na wadau mbalimbali watakaojadiliana kwa pamoja mada zinazohusiana na kaulimbiu ya maadhimisho hayo.