Rais Samia kufanya ziara nchini China

0
20

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia Septemba 02 hadi Septemba 06, mwaka huu ili kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China – Africa Coorperation FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.

Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga imesema katika ziara hiyo, Rais Samia atakutana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping kwa ajili ya mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano mzuri wa kihistoria kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China ulioasisiwa miaka 60 iliyopita.

Miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa pamoja na amani na usalama.

Aidha, Rais Samia anatarajia kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa mkutano wa FOCAC akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.

Mbali na hayo, Rais Samia, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya TAZARA.

Pia, Rais Samia atakutana na makampuni na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Send this to a friend