Mwanariadha wa nchini Uganda, Rebecca Cheptegei (33) amelazwa katika hospitali moja nchini Kenya, baada ya kudaiwa kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake.
Polisi nchini humo wamesema mwanariadha huyo wa mbio za marathon ambaye alishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya hivi majuzi ya Paris, amepata majeraha ya moto katika sehemu kubwa ya mwili wake baada ya kushambuliwa wakati akifanya mazoezi nyumbani kwake Magharibi mwa Kenya.
Mpenzi wake anayedaiwa kumshambulia pia amepata majeraha ya moto, na wote wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Moi mjini Eldoret kwa ajili ya matibabu.
Kamanda wa Polisi kaunti ya Trans Nzoia, Jeremiah Ole Kosiom ameeleza kuwa majirani waliwasikia wapenzi hao wakizozana nje ya nyumba yao na kisha mwanaume huyo alionekana akimmiminia mafuta na kumchoma moto.
Waziri Ndumbaro amuongezea adhabu ya faini Babu wa Tiktok
Ripoti iliyowasilishwa na msimamizi wa Kaunti hiyo imesema kuwa wawili hao walikuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi ambacho kiko karibu na mpaka wa Uganda ambacho Bi Cheptegei alitaka kununua na kujenga nyumba ili kuwa karibu na vituo vingi vya mafunzo ya riadha nchini Kenya.
Bi Cheptegei alimaliza katika nafasi ya 44 kwenye mbio za marathon katika Michezo ya Olimpiki ya hivi majuzi huko Paris, pia alishinda dhahabu kwenye mashindano ya dunia huko Chiang Mai, Thailand, mwaka 2022.