Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano ya CHADEMA

0
39

Jeshi la Polisi limepiga marufuku na kutoa onyo kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha na maandamano ya kudai haki ya watu waliopoteza maisha na watu wasiojulikana yaliyopangwa kufanyika kuanzia Septemba 23, 2024, huku likionya kuwa yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema jeshi hilo linaendelea kufanya upelelezi juu ya matukio hayo baada ya Rais Samia kuelekeza vyombo vya uchunguzi kufanya hivyo kisha kuwasilisha kwake, lakini hatua iliyofikiwa na CHADEMA inawatoa kwenye reli katika upelelezi.

“Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa /kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo, asithubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo yamepigwa marufuku,” ameeleza.

Ameongeza kuwa “ Ikumbukwe kuwa mara kadhaa viongozi na wafuasi wa chama hicho wamekuwa wakipanga na kuharibu mikakati mbalimbali yenye lengo la kuleta vurugu nchini ili kuharibu amani ya nchi yetu kwa sababu wanazozijua wenyewe.”

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wananchi kutokubali kurubuniwa, kudanganywa au kushawishiwa kwa namna yoyote na badala yake waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.