Waziri Mkuu atoa rai kwa viongozi wa dini kusimamia maadili ili kupunguza vitendo viovu

0
4

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wahakikishe wanasimamia na kuimarisha maadili mema kwa jamii ili kuepuka maovu na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.

Ameyasema hayo leo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, Mkoani Geita.

“Nitumie fursa hii kuendelea kutoa rai kwa wananchi, wazazi na viongozi wa dini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wetu katika ngazi zote kwa kuzingatia maadili na tamaduni ya Taifa letu. Ni wajibu wetu kama wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa “Wazazi, ninyi mna jukumu la msingi katika kulea watoto wenu kuanzia katika ngazi ya familia ili kujenga tabia njema, na tukifanya hivyo matendo na hovyo hayatakuwepo, lazima tuwe macho katika matendo haya ambayo yanaweza kuleta hofu kwa jamii yetu.”

Majaliwa amesema kila mmoja ashiriki katika kulinda Taifa kwa kutambua matendo yote yanayoashiria uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa imara “suala la ulinzi na usalama ni letu sote watanzania, ndivyo tulivyofanya tangu Tanzania ipate uhuru.”

Send this to a friend