Rais Samia akemea kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya balozi za kigeni

0
22

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayojitegemea na yenye hadhi, na hivyo haiwezi kuamriwa na watu wa nje kuhusu jinsi ya kuendesha masuala yake ya ndani.

Akizungumza kwenye hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, hafla ambayo pia iliadhimisha miaka 60 ya Jeshi hilo, Rais Samia amekemea vikali kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya balozi za kigeni baada ya kifo cha mwanachama wa CHADEMA, Ali Kibao.

Amefafanua kuwa kauli hizo hazikutolewa kwa ridhaa ya serikali za balozi hizo, na kusisitiza kuwa balozi hizo zinapaswa kuheshimu mamlaka ya Tanzania kama vile balozi za Tanzania zinavyoheshimu mamlaka za nchi nyingine.

Aidha, Rais Samia pia ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuheshimu falsafa yake ya 4R’s (Maridhiano, Uvumilivu, Haki na Uwajibikaji) na kutochukulia kimzaha uhuru wa kisiasa wanaoufurahia sasa.

“R4 si sababu ya utovu wa nidhamu, si sababu ya kukiuka sheria za nchi sheria za nchi zipo pale pale, ni vizuri wasisahau mapito waliyopita. Serikali imejitahidi sana kurejesha uhuru wa vyama vya siasa,uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa raia kwa ujumla.

Wale waliokuwa uhamishoni walirejea nchini, waliokuwa na kesi za jinai na wengine tulizifumbia macho, waliokuwa jela tuliwatoa sasa wapo huru na wanaendelea na shughuli zao ikiwamo shughuli za kisisasa, lengo letu likiwa kuwaleta watu pamoja ili tuweze kujenga nchi yetu,” ameeleza.

Mbali na hayo, Rais Samia amewapongeza Askari Polisi kwa kazi yao kubwa ya kulinda amani na utulivu wa taifa.