Tanzania ya kwanza Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa usalama mtandaoni

0
44

Tanzania imeshika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa usalama wa mtandaoni, kwa mujibu wa Ripoti ya Kielezo cha Usalama wa Mtandao ya mwaka 2024 (GCI).

Tanzania imepata alama ya asilimia 100 katika nguzo zote tano za usalama wa mtandaoni, ambazo ni: kisheria, kiteknolojia, kiutawala, ushirikiano na kujenga uwezo.

Kimataifa, Tanzania imewekwa kwenye kundi la Tier 1 – mfano wa kuigwa, kundi la juu zaidi pamoja na nchi kama Marekani, Uingereza, na Korea Kusini. Kundi hili limetengwa kwa ajili ya mataifa ambayo yanaonyesha kufanya vyema kwenye nguzo zote tano za usalama wa mtandaoni, na ni nchi 46 tu duniani zikiwemo nchi tano kutoka Afrika, zimefikia heshima hii.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, amesisitiza kujitolea kwa mamlaka hiyo katika kuhakikisha mazingira salama ya mtandao, kwa kushirikiana na nchi jirani.

Ripoti ya GCI, iliyotathmini nchi 194, inalenga kusaidia mataifa kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa na kuhimiza kujenga uwezo katika usalama wa mtandao.