Watatu mashuhuri akiwemo Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Rais wa Benin wamekamatwa kwa tuhuma za kupanga jaribio la mapinduzi nchini humo.
Waendesha mashtaka wa Benin wamesema wengine wanaotuhumiwa kupanga jaribio hilo la mapinduzi ni waziri wa zamani wa michezo na mfanyabiashara aliye karibu na Rais Patrice Talon.
Mwendesha mashtaka kwenye mahakama ya uhalifu wa kifedha na ugaidi nchini Benin, Elonm Mario Metonou amesema njama hiyo ya mapinduzi ilikuwa imepangwa kutekelezwa siku ya Ijumaa Septemba 27, mwaka huu.
Mahakama imesema Waziri wa zamani, Oswald Homeky alikamatwa Jumanne wakati akimkabidhi kamanda Djimon Dieudonne Tevoedire dola milioni 2.5, [sawa na TZS bilioni 6.84].
Mfanyabiashara Olivier Boko, anayejulikana kama rafiki wa muda mrefu wa Rais Patrice Talon, alikamatwa usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne katika mji mkuu wa Benin, Cotonou, mahakama imeeleza.