Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi ameagiza Polisi wilayani Maswa kuondoka na wananchi wawili waliotoa tuhuma za kuwepo kwa vitendo vya utekaji, kupotezwa na kuuawa watu wazima na watoto lakini wakashindwa kuthibitisha tuhuma hizo ili kupata maelezo ya kina kutoka kwao.
Hayo yamejiri baada ya wakazi wa vijiji vya Sangamwalugesha na Mbaragane kutoa malalamiko mbele yake wakidai hali ya ulinzi na usalama kwenye vijiji vyao si shwari kwa kuwa kuna vitendo vya watoto na watu kupotea, kutekwa na kuuawa na kupelekea wananchi kuishi kwa mashaka.
“Hapa Sangamwalugesha tuna shida, roho ziko hatihati, wananchi wanaishi kwa mashaka ikifika jioni saa 12.00 unakaa ndani na mtoto kwa kuhofia vitendo vya kutekwa, kupotezwa na kuuawa wakati Jeshi letu la Polisi lipo lakini maisha yetu yana dukuduku,” amesema Festo Mikael wakati akitoa maoni mbele ya Mkuu wa Mkoa
Baada ya malalamiko hayo, RC Kihongosi alimtaka mwananchi huyo kuthibitisha kauli hiyo lakini alishindwa, ndipo alipowauliza wananchi kama matukio hayo yapo, ambao nao walikana kuwa hakuna matukio hayo katika Kijiji hicho.
Naye mkazi mwingine aliyetambulika kwa jina la Costantine Samo mkazi wa Kijiji cha Mbaragane amedai kuwepo kwa matukio ya watu kuuawa na kutolewa nyongo, hivyo kumtaka Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Simiyu na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Maswa kutoa maelezo ya kina juu ya kuwepo kwa matukio hayo, na alipotakiwa kuthibitisha taarifa hizo alishindwa pia.
Kihongosi alimuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Maswa, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP), Maganga Ngosha kuwachukua wanananchi hao kwa ajili ya kupata maelezo ya kina.
Chanzo: Mwananchi