Dkt. Nchemba aishukuru IMF kwa misaada na mikopo nafuu nchini

0
6

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia misaada na mikopo nafuu inayoipatia Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Amesema hayo Jijini Dodoma, wakati akifungua vikao vya majadiliano kati ya Serikali na timu ya wataalam kutoka IMF, iliyowasili nchini kufanya Tathimini ya Awamu ya Nne ya utekelezaji wa Program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na Awamu ya kwanza ya Programu ya Resilient and Sustainable Fund (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Tanzania inatekeleza Programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Programu hiyo ya RSF baada ya kukidhi vigezo kufuatia uongozi wa Rais Samia Suluhu ambaye ni kinara wa masuala ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

‘‘Baada ya kutekeleza kwa mafanikio programu nyingine zilizopita ikiwepo ile ya Dirisha la Dharura ambapo tulipata fedha za kukabiliana na athari za UVIKO-19 (Rapid Credit Facility- (RCF)), na huu wa ECF unalolenga kufufua na kuimarisha uchumi, Tanzania imetimiza sifa ya kutekeleza programu ya RSF ambapo tutapata fedha za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka IMF,’’ alisema Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa IMF, Charalambos Tsangarides amesema shirika hilo limeridhishwa na utekelezaji wa programu ya ECF ambayo utekelezaji wake utakamilika katika mwaka wa fedha 2025/2026 na kuipongeza Tanzania kwa kupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo kutekeleza programu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Send this to a friend