Chama cha ACT- Wazalendo kimelaani hatua ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha leseni ya huduma za maudhui mtandaoni kwa kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayojumuisha Mwananchi Digital, The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti kwa kipindi cha siku 30.
Katika taarifa iliyotolewa na Chama hicho kwa umma imesema taarifa hiyo ni tishio na inaashiria kuendeleza mazingira kandamizi kwa vyombo vya Habari ili visifanye kazi zao kwa uhuru kupitia vifungu kandamizi vinavyotumiwa kuzima uhuru wao.
”ACT Wazalendo tunapinga vikali kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi mtandaoni na kuitaka Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuondoa zuio hilo ili gazeti liendelee kutoa huduma ya Habari kwa umma,” imesema ACT Wazalendo.
Aidha, imesema matukio ya kukamatwa kwa waandishi, kuzuiwa kwa vyombo vya Habari na kufungiwa kwa Mwananchi inaonesha bado uhuru wa habari haujaimarika, hivyo kutoa wito kwa Watanzania kusimama kwa pamoja, kutetea na kulinda uhuru wa vyombo vya Habari na waandishi na habari.
Katika taarifa iliyotolewa na TCRA Oktoba 02, 2024 imesema kuwa kampuni hiyo ilichapisha maudhui yaliyokiuka kanuni ambayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa.