Waziri Mkuu aagiza watumishi Kigamboni wafikishwe mahakamani kwa ubadhirifu 

0
32

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameelekeza kufikishwa mahakamani mara moja kwa maafisa wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na watumishi wanne wa kitengo cha Akaunti Jumuifu ya Amana (TSA) kilichopo TAMISEMI kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 165.6.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam katika ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo amefikia maamuzi hayo kutokana na uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda kufuatilia tuhuma za ubadhirifu huo pamoja na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kujiridhisha na ukweli wa tuhuma hizo.

Waziri Mkuu amesema kuwa matokeo ya timu ya uchunguzi aliyoiunda yalionesha kuwa watumishi hao walikuwa wanatumia akaunti ya Amana kuficha fedha hizo tofauti na malengo ya matumizi ya akaunti hiyo.

Amesema watumishi watatu wasio waaminifu kutoka TAMISEMI walishirikiana na watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kuleta shilingi milioni 165.6 na kuzihifadhi kwenye akaunti ya Amana na zikakaa mwaka mzima bila Mkurugenzi, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Idara wengine kujua.

Waziri Mkuu amesema kuwa walianza kutumia fedha hizo bila kulijulisha Baraza la Madiwani na bila kuingizwa kwenye bajeti ya Halmashauri ili wakuu wengine wa idara wajue kwamba kuna fedha, na baada ya mtandao huo kujulikana, timu ya uchunguzi ilifika katika Halmashauri hiyo na kumhoji Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Erasto Kiwale ambaye alikiri kutofahamu kuhusu uwepo fedha hizo.

“Mkurugenzi alimuuliza Mkuu wa Kitengo cha Fedha cha Halmashauri, Geofrey James Martin ambaye alikiri kuwepo kwa fedha hizo na Mkurugenzi alimtaka kuzirejesha zilipotoka kwa kuwa hazikuwa na maelezo ila Geofrey Martin hakufanya hivyo na alipokuja kuhojiwa na timu ni kwa nini hakuzirejesha alisema fedha hizo zimetumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya MDH (Management and Development for Health) lakini hata Mganga Mkuu wa Wilaya hafahamu kama ameletewa fedha,” amesema

Amesema kuwa fedha hizo zilianza kufanyiwa matumizi ambapo milioni 105.6 zililipwa kwenye maboresho ya barabara inayoelekea dampo la Lingate. “Fedha hizi zililipwa mara tatu, ambapo shilingi milioni 77.5 alilipwa mzabuni anayeitwa Konya Investiment Company Ltd, shilingi milioni 28.1 zililipwa kwa mzabuni anaitwa Mbogolo Investiment Company na shilingi milioni 2.4 ilikuwa ni posho ya msimamizi.”

Majaliwa amesema kuwa timu ya uchunguzi ilipotembelea eneo la mradi na kumhoji mkuu wa mradi, Godwin Cheyo ambaye alisema ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa ni wa udongo badala ya changarawe na gharama zote za mradi hazikuzidi milioni 30 na kwamba wazabuni waliotekeleza mradi hawakuwa na sifa na walitumika tu kupitishia fedha.

Send this to a friend