Mfahamu Naibu Rais Gachagua na kwanini Wakenya wanataka kumuondoa madarakani

0
30

Mwanasiasa aliyepitia kwenye taasisi ya mafunzo ya Upolisi mwaka 1990 baada ya kuhitimu Shahada ya Sanaa ya Sayansi ya Siasa na Fasihi mwaka 1988 na kisha Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Rigathi Gachagua (59) anakabiliwa na shinikizo la kuondolewa madarakani kama Makamu wa Rais ikiwa ni takriban miaka miwili tangu kuanza kuhudumu nafasi hiyo.

Chimbuko la Gachagua ni kabila la Wakikuyu, eneo maarufu la Mlima Kenya ambalo lilitazamwa zaidi na wagombea wa Urais mwaka 2022, William Ruto na aliyekuwa kiongozi wa chama cha Orange Demcratic Movement (ODM), Raila Odinga, huku uamuzi wa Rais Ruto kumchagua Gachua kuwa Makamu wake ukielezwa kuwa ni kutokana na Gachagua kutoka Mlima Kenya.

Akiwa na uzoefu mbalimbali kwenye sekta ya uongozi kama; msaidizi mkuu wa waziri wa masuala ya umma mwaka 1991, mkuu wa wilaya ya Laikipia mwaka 1997 hadi 1999, msaidizi binafsi wa aliyekuwa Rais, Uhuru Kenyatta, Gachagua aliingia madarakani kwenye nafasi ya juu kama Naibu Rais wa Kenya.

Ndani ya miaka miwili akiwa kama Naibu wa Rais, Gachagua amekuwa akishtumiwa kwa kuwa mkabila, huku wakosoaji wakidai kuwa kama Naibu wa Rais haichukulii ofisi yake kama ya kitaifa ili kuwaunganisha Wakenya, bali anatoa upendeleo zaidi kwa watu wa Mlima Kenya, jamii ya Kikuyu anayotoka, akidaiwa pia kuchochea chuki za kikabila, ufisadi na kuidhoofisha serikali.

Tofauti kati ya Rais Ruto na Gachagua zimeongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya kuhusishwa kuhusika kwenye mipango ya maandamano ya vijana ya kuipinga Serikali mapema mwaka huu, jambo ambalo Gachagua alikanusha shutuma hizo.

Pia, Gachagua amelaumiwa na washirika wa Rais Ruto kwa kuhutubia taifa kupitia runinga akimshtumu Mkuu wa Idara ya Ujasusi, Noordin Hajji kwa kutoipa serikali taarifa za manung’uniko ya wananchi kuhusu mapendekezo ya kuwakata ushuru yaliyokuwa katika mswada wa Fedha wa 2024/25.

Hata hivyo, Gachagua amewashtumu washirika na wasaidizi wa Rais Ruto kwa kuwa na hila dhidi yake, akisema kuwa hila hizo zinakuja kwa sababu yeye ni msema kweli, kwamba msimamo wake wa kuwaambia Wakenya ukweli ndio unaopelekea kupigwa vita. Pia amelalamika kudharauliwa, kutukanwa na kufichwa kuhusu mipango ya serikali na hata kuzuiwa kumfikia Rais.

Baadhi ya wachambuzi wamedai kuwa Rais Ruto na washirika wake hawajafurahia maneno ya kila mara ya Gachagua kwamba ni eneo la Mlima Kenya ndilo lililompigia kura Rais Ruto kwa wingi na kumpa ushindi.

Wabunge nchini Kenya wanaendelea na mchakato wa kumuondoa madarakani Gachagua baada ya wabunge 291 kutia Saini muswada wa kumuondoa, wakisema kuwa kiongozi huyo ameenda kinyume na kiapo chake.

Wabunge wamewasilisha mashtaka 11 yanayomkabili Gachagua, ikiwa ni pamoja na kikiuka katiba, kuipinga serikali, kueneza ukabila na kujipatia mali kinyume cha sheria.

Mvutano kati ya Rais wa Kenya na Naibu wake sio jambo geni nchini Kenya, kwani Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta alifungua ukurasa huo na Makamu wake wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Jaramogi Oginga. Pia Rais aliyetangulia, Uhuru Kenyatta aliingia kwenye mgogoro mkubwa na Naibu wake, William Ruto Katika muhula wa pili.

Send this to a friend