Watumishi 108 kutoka ofisi ya Gachagua wapewa likizo ya lazima
Serikali imewapa likizo ya lazima watumishi wote 108 walioko katika ofisi ya Naibu Rais wa Kenya aliyeondolewa madarakani, Rigathi Gachagua kuanzia leo Jumamosi, Oktoba 18.
Katika barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Utawala, Patrick Mwangi, wakuu wote wa idara wameagizwa kuhakikisha wanateua afisa anayehusika kuchukua majukumu mara moja.
Waraka huo pia umeeleza kwa kina orodha ya watumishi 108 ikiwa ni pamoja na majina yao, namba za watumishi, vyeo vya kazi na madaraja ya kazi huku miongoni mwa majina maarufu ni Njeri Rugene, Mshauri wa Mawasiliano katika Huduma ya Mawasiliano ya Naibu Rais (DPCS), pamoja na Rose Wangari Gakuo, Katibu wa Shughuli za Kitaifa.
Siku moja baada ya kutolewa uamuzi wa kumwondoa Gachagua, Rais William Ruto aliwasilisha jina la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki kwa Bunge la seneti kama Naibu Rais aliyeteuliwa, ambapo bunge lilimuidhinisha kwa kauli moja.
Hata hivyo, mahakama ilimpa Gachagua fursa ya pili kwa kusimamisha uamuzi wa Seneti wa kumwondoa madarakani na kumzuia Kindiki kuchukua nafasi hiyo hadi October 24,2024 kesi hiyo itakaposikilizwa na jopo la majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu, Martha Koome.