Serikali: Wananchi milioni 26.7 wamejiandikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa

0
23

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya wapiga kura 26,769,995 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, sawa na asilimia 81.15 ya lengo la kuandikisha watu 32,987,579.

Akianisha mikoa mitano yenye asilimia kubwa ya uandikishaji hadi kufikia Oktoba 18, 2024, Waziri Mchengerwa amesema mkoa wa Tanga umefikia asilimia 101.13 ya malengo, mkoa wa Pwani umefikia asilimia 98.74, Mwanza asilimia 94.09, Dar es Salaam asilimia 86.66, na Dodoma umefikia asilimia 80.63 ya malengo.

“Mpaka Oktoba 19, 2024, jumla ya uandikishaji kwa wanaume ni 13,033,988 sawa na asilimia 48.69 na wanawake ni 13,736,007 sawa na asilimia 51.31 ya watu wote waliojiandikisha kuanzia tarehe 11 hadi 19 Oktoba, 2024”, amesema Mchengerwa.

Ameongeza, “Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote waliojitokeza kujiandikisha hadi muda huu ninaotoa tathmini ya uandikishaji, kwani tayari wamejiwekea mazingira kukubalika kisheria ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa wanaowataka ifikapo tarehe 27 Oktoba 2024.”

Zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lilizinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hasan aliyejiandilkisha katika Kitongoji chake cha Sokoine Kijiji cha Chamwino Oktoba 11, mwaka huu.

Send this to a friend