Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema Watanzania milioni 31,282,331 wamejiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ikiwa ni sawa na asilimia 94.83 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa amesema kati ya Watanzania waliojiandikisha, wanaume ni milioni 15,236,772 Sawa na asilimia 48.71 huku wanawake wakiwa milioni 16,045,559 Sawa na asilimia 51.29.
“Matokeo haya yanaonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 ambapo waliandikishwa wapiga kura milioni 19,681,259 tu sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandisha wapiga kura takriban 22,916,412,” amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na uwekezaji mkubwa wa uelimishaji na uhamasishaji katika ngazi zote muhimu, huku akiwapongeza wananchi waliojitokeza kujiandikisha kwakuwa tayari wamepata sifa ya kisheria ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Aidha, Waziri Mchengerwa amewaelekeza wananchi waliojiandikisha kujitokeza kuhakiki orodha ya majina kwenye vituo kuanzai Oktoba 21 hadi Oktoba 27, mwaka huu na kutoa rai kwa wananchi wanaotaka kugombea kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 1 ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba katika uchaguzi huo.