Rostam: Tanzania kuichagua DP World kuendesha bandari lilikuwa chaguo bora zaidi
Mwenyekiti wa Taifa Group Ltd, Rostam Aziz amesema Tanzania kuichagua kampuni ya DP World lilikuwa ni chaguo bora zaidi kutokana na ufanisi na rekodi nzuri iliyonayo kampuni hiyo katika usimamizi wa badari.
Ameyasema hayo kwenye mjadala wa jukwaa la Mkutano wa Kilele wa Financial Times Africa uliofanyika London, ambao ulihudhuriwa na wakuu wa nchi, Magavana wa Mabenki Kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mawaziri wa Uingereza, IMF, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, mabenki, na wadau wengine.
“Tanzania iko katika eneo nzuri kijiografia, ina nchi saba zinazozunguka, na nchi zote hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam. Sasa, uzoefu wetu na uendeshaji wa bandari kabla ya hili umekuwa wa kusikitisha, na ufanisi umekuwa wa kiwango cha chini sana. Tumekuwa na meli zinazongoja kwa muda mrefu bandarini, jambo ambalo linagharimu sana watumiaji wa mwisho na uchumi kwa ujuma.
Ikiwa utaenda Dar es Salaam na kutazama baharini, utaona kama vile kuna miti mingi ya Krismasi kutokana na meli nyingi zinazongoja kutia nanga. Hivyo basi, tulihitaji kutafuta mwendeshaji mwenye uzoefu, rekodi nzuri, na maslahi kijiografia kuhusu Dar es Salaam, na tulipofanya tathmini tuliona kwamba DP World ndiyo mshirika bora zaidi tunaweza kuwa naye,” amesema.
Aidha, amesema kuwa “Hapo awali tuliwahi kuikabidhi sehemu ya bandari kwa Hutchison kutoka Hong Kong. Na kwa sababu tuko mbali sana kijiografia na Hong Kong, na tofauti ya wakati, nadhani walijali kidogo sana kuhusu Dar es Salaam na hakukuwa na maboresho makubwa kwenye ‘terminal’ hiyo iliyokuwa chini ya Hutchison.”
Rostam pia ametumia jukwaa hilo kuzungumzia changamoto zinazokabili nchi za Afrika katika kupata mikopo yenye riba nafuu, ambapo ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa na makampuni ya fedha kuacha ubaguzi wa kijiografia dhidi ya Afrika na kuweka viwango vya riba sawa na maeneo mengine duniani, pamoja na kutoa wito kwa nchi zilizoendelea za G7 na mashirika ya kibenki kuweka sera ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Afrika.