Rwanda yatangaza kutosajili pikipiki za abiria zinazotumia petroli ifikapo mwakani

0
51

Serikali ya Rwanda imetangaza kuwa kuanzia mwaka ujao 2025, haitasajili tena pikipiki za petroli zinazotumika kusafirisha abiria (bodaboda), katika jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.

Waziri wa Miundombinu, Jimmy Gasore, ameeleza kuwa lengo ni kutumia nishati yenye ufanisi zaidi na kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochafua mazingira.

Sheria hii mpya itaanza kutumika jijini Kigali na itahusisha pikipiki zinazotumika kubeba abiria nchini Rwanda, ikiwa ni usafiri mkuu nchini humo. Hii ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuimarisha usafiri wa umeme kwa kuleta afueni kwa wamiliki na watoa huduma katika sekta hii.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara, Rwanda ina takriban pikipiki 110,000, huku 30,000 zikiwa Kigali, na kati ya hizo, 70,000 hutumika kubeba abiria. Rwanda imeshatoa ruzuku mbalimbali ili kufanikisha mpango huu wa umeme, ikiwemo punguzo la bei ya umeme kwa malipo ya kuchaji betri pamoja na msamaha wa kodi kwa makampuni yanayozalisha betri.

Kampuni za ndani zinazouza pikipiki za umeme, kama SAFI Universal Link, zimepongeza hatua hii, ambapo Meneja wa SAFI, Eve Kayiranga, amesema kuwa, “Sera hii sio tu inapunguza uzalishaji wa kaboni lakini pia inaonesha maendeleo yaliyopatikana katika kujenga miundombinu inayounga mkono usafiri wa umeme nchini Rwanda.”

Send this to a friend