Maboresho mradi wa BRT awamu ya kwanza Dar kugharimu shilingi bilioni 18

0
24

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam imesema inatekeleza mradi wa matengenezo ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza chini ya mradi wa OPBRC (Output and Performance-Based Road Contract) uliosainiwa rasmi Septemba 07, 2018.

Mradi huo wa muda mrefu, ulianza rasmi Aprili 01, 2019 ukitekelezwa na mkandarasi M/s Bharya Engineering & Contracting Co. Ltd (BECCO) kwa utekelezaji wa muda wa miezi sitini (60) yaani miaka mitano.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi John Mkumbo leo na kueleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 18.509 ambazo zinajumuisha makundi matatu ya kazi.

Ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na mradi wa matengenezo ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 21.4 ikihusisha: Barabara ya Morogoro kuanzia Ferry mpaka Kimara Mwisho, Barabara ya Kawawa (Magomeni Mapipa – Morocco); na Barabara ya Msimbazi (Fire – Msimbazi BRT Station).

Mhandisi Mkumbo amesema TANROADS pia inatekeleza kazi za maboresho ya sehemu zilizoharibika ikihusisha matengenezo makubwa ya tabaka la lami katika sehemu zilizokuwa zimeharibika.

Pia TANROADS imesema imefanya kazi za dharula zikihusisha matengenezo ya uharibifu ambao haukutarajiwa. Kazi hizi ni pamoja na; Kuondoa tope, mchanga na takataka kwenye daraja na eneo la barabara wakati wa mafuriko na mvua kubwa, na matengenezo ya miundombinu yatokanayo na ajali za barabarani kwenye miundombinu ya BRT awamu ya kwanza.

Send this to a friend