Kampuni 10 za wazawa zadai kusitishiwa mikataba na kampuni ya madini bila taarifa

0
17

Kampuni kumi za wazawa nchini Tanzania zinazotoa huduma kwa Shanta Mine zimetoa malalamiko kuhusu mikataba yao kusitishwa bila sababu za msingi, huku wakidai kuwa ni takriban miezi mitatu hawajapata kazi mpya (zabuni).

Akizungumza na gazeti la Nipashe Jumatatu Novemba 4, 2024, mmoja wa wamiliki wa kampuni hizo (jina lilihifadhiwa na gazeti hilo) amesema kuwa wamepata taarifa zisizo rasmi kuwa kampuni zao zimeondolewa kwenye orodha ya zabuni za Shanta Mining.

“Sisi tunatambulishwa hadi kwenye Tume ya Madini kwamba tunaiipa huduma kampuni hiyo, maana sheria za nchi zinaelekeza kampuni za madini zinazohitajika kutumia vifaa au huduma inayozidi Dola 100,000 lazima mikataba ipatikane kupitia Tume ya Madini”, ameeleza mmiliki huyo na kuongeza,

“Tunashangaa kampuni zetu zimeondolewa kwenye orodha ya kupewa kazi za Shanta. Sasa kazi zote anapewa… (akataja jina la kampuni). Tunajua kampuni hii imesajiliwa Tanzania, lakini wamiliki wake wana asili ya India”.

Ameendelea kudai kuwa hatua iliyochukuliwa ya kuwanyima kazi wazawa, wanahisi italeta madhara si tu kwa kampuni zao, bali hata katika mapato ya madini kutokana na ukiukwaji utaratibu wa ‘local content’ [kutumia wazawa au kampuni za wazawa katika kupata huduma au vifaa].

Katika kulijibia hilo, Mkuu wa Operesheni wa Shanta Mining, Honest Mrema, aliliambia Nipashe kuwa Shanta Mining bado haijachukua hatua yoyote ya kusitisha huduma kwa kampuni za wazawa, bali wameanzisha mchakato wa kuchunguza madai ya udanganyifu wa kifedha kwa baadhi ya watoa huduma.

“Hivi karibuni, Shanta imekuwa inaendelea na ukaguzi wa ununuzi na baadhi ya masuala kuhusu ubora, bei na udanganyifu wa kifedha umegundulika. Kazi hii bado inaendelea na ripoti kamili itakapotolewa itawasilishwa pia kwa Tume ya Madini. Kwa sasa, baadhi ya malipo yamezuiwa hadi matokeo ya uchunguzi yatakapojulikana”, ameeleza Mrema.

Aidha amesema kutokana na changamoto hizo, baadhi ya wauzaji wao (alitaja majina ya kampuni mbili) wameathirika, na majadiliano yanaendelea kutafuta suluhisho, na akaongeza kuwa Shanta imejizatiti kutumia wauzaji wa ndani na inahakikisha inazingatia kikamilifu kanuni za ‘local content’.

Alipoulizwa kuhusu kampuni inayolalamikiwa kwamba hivi sasa wanaendelea kuipa kazi/ zabuni ilihali wazawa wengine wananyimwa, alisema “si kampuni zote zinatiliwa shaka, zipo nyingine zaidi zinaendelea na kazi”.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipotafutwa na Nipashe siku ya Jumanne Novemba 5, 2024 kuzungumzia suala hilo, alisema hakuwa na taarifa za kinachojiri katika katika Kampuni ya Shanta.

Waziri Mavunde alithibitisha kuwa wizara inachukua hatua za haraka kuchunguza malalamiko hayo na alieleza kuwa ameelekeza timu yake ifanye uchunguzi wa kina ili kujiridhisha juu ya usahihi wa taarifa zilizotolewa.