TAMISEMI: Wagombea ambao hawajaridhishwa na uteuzi waweke pingamizi

0
9

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waweke pingamizi ndani ya siku 2 kuanzia Novemba 08 hadi 09, 2024.

Mchengerwa ameeleza kuwa pingamizi hilo linaweza kuwasilishwa kwa maandishi ndani ya siku mbili tangu uamuzi au uteuzi ulipofanyika, ambapo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atalishughulikia pingamizi hilo na kutoa uamuzi ndani ya siku mbili tangu alipolipokea.

“Mara baada ya uteuzi kukamilika, majina ya wagombea wenye sifa na wale ambao hawajakidhi vigezo vya kugombea yatabandikwa hadharani ili umma uweze kuyapata wakiwemo wagombea wenyewe.

Kuanzia leo tarehe 8 na kesho tarehe 9 Novemba 2024, kwa mgombea yeyote ambaye hatoridhika na uamuzi wa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhusu uteuzi, anapaswa kutumia nafasi ya siku hizi mbili ili malalamiko yake yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni,” amesisitiza.

Serikali: Asilimia 94.83 wamejiandikisha daftari la Wapiga Kura

Ameongeza kuwa iwapo mgombea hatoridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi juu ya pingamizi lake, ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ndani ya muda usiozidi siku nne baada ya uamuzi huo kutolewa. Maana yake Rufaa ziwasilishwe kuanzia Novemba 10 hadi 13, 2024 kwa kamati ya Rufaa.

Aidha, amesema ni muhimu wagombea wote wafuate taratibu za kisheria na kuhakikisha malalamiko yao yanawasilishwa katika sehemu sahihi ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ili kusaidia kuimarisha utulivu na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Send this to a friend