Waziri Mkuu ahimiza viongozi wa vyama vya siasa kudumisha amani uchaguzi wa Serikali za Mitaa

0
10

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa vinara katika kulinda amani na kukemea viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.

“Hamasisheni wanachama wenu kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia kudumisha amani iliyopo. Wananchi wote waliojiandikisha katika orodha ya wapiga kura wa uchaguzi wa mamlaka za Serikali za Mitaa wajitokeze kwa wingi kupiga kura katika vituo vyao siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024. Siku hiyo itakuwa ya mapumziko maalum kwa ajili ya uchaguzi huo,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Jumapili, Novemba 10, 2024 wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu na Kongamano la Umuhimu wa Amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amewasihi Watanzania na viongozi wa dini kuendelea kuitangaza amani ndani na nje.”

Katika Kongamano hilo, ambalo linaratibiwa na Jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Tanzania, Waziri Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi hao kuhamasisha wanachama wao kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia suala la kudumisha amani kwa muhimu mkubwa.

Aidha, amesisitiza kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ajitokeze kupiga kura ili kuwachagua vongozi ambao ni mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa. “Ikumbukwe kuwa kupiga kura ni wajibu na haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na madhehebu ya dini pamoja na taasisi zote, ambapo licha ya kutoa mafundisho ya kiroho, taasisi za dini zimekuwa zikiunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.