Mabelya: Wananchi wako tayari kupokea mikopo ya asilimia 10 ili kujikomboa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, ameeleza kwamba mpango mpya wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu utaimarisha usalama wa fedha za serikali huku ukihakikisha marejesho yanafanyika kwa ufanisi.
Mabelya ametoa kauli hiyo leo Novemba 11, 2024, katika Kongamano la Uelimishaji na Uhamasishaji Jamii Juu ya Uwepo wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Sambamba na Matumizi ya Nishati Safi linalofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.
Katika hotuba yake, Mabelya ameeleza kwamba miaka ya nyuma utoaji wa mikopo kupitia halmashauri ulikumbwa na changamoto nyingi, hususan katika urejeshaji wa mikopo hiyo, akieleza kuwa wajasiriamali walikuwa wakijiunga kwenye vikundi lakini walishindwa kudumisha biashara zao, na hivyo kukumbwa na madeni makubwa ambayo yaliathiri sio tu maisha yao binafsi bali pia familia zao.
“Mwisho wa siku, mkopo ni lazima urejeshwe, na changamoto hizo zimekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wetu,” amesema Mabelya.
Kwa kutambua changamoto hizo, Mabelya amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliona haja ya kuleta mabadiliko katika utaratibu wa utoaji wa mikopo hii, ambapo sasa, mikopo hiyo itatolewa kupitia benki badala ya mfumo wa awali uliotumia halmashauri moja kwa moja.
“Kwa halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala, tumeteuliwa kuwa miongoni mwa halmashauri 10 za mfano nchini, ambapo mikopo hii sasa itatolewa kwa njia ya kibenki. Hatua hii inalenga kulinda fedha za serikali na kuimarisha utaratibu wa marejesho,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa mfumo huo mpya pia unatoa uhakika kwamba mkopaji ni mshiriki halali wa vikundi vilivyoidhinishwa, huku utaratibu wa marejesho ukiwa wazi zaidi ili kuepusha madeni yasiyolipika. “Tangu mwezi Julai mwaka huu, dirisha la utoaji mikopo limefunguliwa rasmi. Tumefanya mafunzo kwa wataalamu wetu na kwa wananchi katika kata zote 36 za Wilaya ya Ilala,” amesema.
Mabelya ameelezea zaidi kwamba mafunzo hayo yamekuwa yakifanyika katika ngazi ya kata ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mzuri kuhusu matumizi ya mikopo hiyo.