Baada ya taarifa ya Chama Cha ACT Wazalendo kudai kuwa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo kutekwa leo asubuhi, Jeshi la Polisi limesema kiongozi huyo alikamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa na gari aina ya Landcruiser nyeupe yenye usajili namba T249 CMV.
Taarifa ya Polisi imesema mashuhuda wameeleza kuwa katika purukushani za ukamataji, begi dogo lilidondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo vimetambuliwa kuwa ni vya Abdul Omary Nondo.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza mara baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo Polisi sambamba na kufungua jalada.
Kiongozi huyo anadaiwa kukamatwa muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi katika kituo cha mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma kwaajili ya kushiriki shughuli za chama hicho.