Wanaofanya kazi ya ngono nchini Ubelgiji kupata haki sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine

0
4

Wafanyakazi wa ngono nchini Ubelgiji sasa wanapata ulinzi sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine kupitia sheria mpya ya kihistoria iliyopitishwa mwezi Mei mwaka huu na kuanza kutekelezwa siku ya Jumapili.

Sheria hiyo inatoa haki za ajira rasmi, ikiwemo likizo ya uzazi, bima ya afya, posho za ukosefu wa ajira, na malipo ya ugonjwa.

Kwa mujibu wa Quentin Deltour, Meneja wa Mahusiano ya Umma wa shirika la Espace P linalotetea haki za wafanyakazi wa ngono, sheria hiyo ni hatua ya kwanza ya aina yake duniani inayotoa mfumo wa kisheria kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi wa ngono.

Sheria hiyo inatoa haki za kipekee kwa wafanyakazi wa ngono, kama vile uwezo wa kukataa kutoa huduma kwa mteja au kutekeleza kitendo chochote cha kingono ambacho hawakubaliani nacho. Pia, wafanyakazi wanaruhusiwa kusitisha shughuli yoyote wakati wowote wanapojisikia kufanya hivyo.

Mbali na haki hizo, waajiri wa wafanyakazi wa ngono wanatakiwa kuomba leseni rasmi kutoka serikalini kabla ya kuendesha shughuli zao. Masharti ya kupatiwa leseni yanajumuisha kutokuwa na rekodi ya makosa kama ubakaji au biashara haramu ya binadamu.

Sheria mpya pia inaweka majukumu kwa waajiri, yakiwemo kutoa vifaa muhimu kama kondomu, shuka safi za kitanda, na kuweka kitufe cha dharura kwenye vyumba vya wafanyakazi ili kuongeza usalama wao.

“Hii ni mara ya kwanza duniani ambapo mfumo wa kisheria wa kina unatoa haki sawa kwa wafanyakazi wa ngono kama wafanyakazi wa sekta nyingine na kuwahakikishia ulinzi dhidi ya hatari zinazotokana na kazi hii,” amesema Daan Bauwens, Mkurugenzi wa Muungano wa Wafanyakazi wa Ngono wa Ubelgiji.

Ameongeza kuwa Sheria hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa ngono, kuwawezesha kupata ulinzi wa kijamii na kuhakikisha kuwa kazi zao zinafanyika kwa heshima na usalama.

Send this to a friend