Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametangaza hatua muhimu zinazofuata katika mchakato wa kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 baada ya uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Dira hiyo uliofanyika leo ukiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo amebainisha kuwa mchakato wa kukamilisha Dira ya Taifa utapitia hatua tano muhimu zinazolenga kukusanya maoni zaidi ya wananchi, kuyahakiki, na kuyajumuisha kwenye Dira. Hatua hizo zitahusisha maoni ya wananchi na wadau mbalimbali, mijadala ya vyombo vya serikali, na hatimaye mjadala wa bunge kabla ya Dira hiyo kuidhinishwa rasmi.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila, maoni mapya yataanza kukusanywa Desemba 14, 2024 kupitia hatua ya uhakiki ya Rasimu ya Dira, na shughuli hiyo itahitimishwa Januari 14, 2025, ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atapokea Rasimu ya Pili iliyoboreshwa.
Baada ya hapo, maamuzi ya Serikali yatafanyika kupitia Makatibu Wakuu, Tume ya Taifa ya Mipango, na Baraza la Mawaziri. Hatua ya mwisho ya mchakato huu itakuwa kuwasilisha Rasimu hiyo Bungeni kati ya Aprili na Mei 2025 kwa ajili ya majadiliano na uidhinishaji rasmi.
Hatimaye, Rais Samia Suluhu anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kati ya Mei na Juni 2025, kulingana na ratiba yake.
Profesa Mkumbo amesisitiza kuwa Dira hiyo ni mali ya wananchi, na mchakato mzima unalenga kuhusisha maoni yao kwa kiwango kikubwa, kuhakikisha kuwa ndoto za maendeleo ya nchi zinazingatia matamanio na matarajio ya makundi yote ya jamii.