Rais Dkt. Mwinyi azindua Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025

0
24

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema malengo makuu ya Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ni kugusa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki pamoja na kuwa na Dira jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa Rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Zanzibar, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameiagiza timu kuu ya wataalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu ili kuwa na Dira yenye kubeba maono ya wananchi wote.

Vilevile Rais Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo kwa vyombo mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.

Halikadhalika Dkt. Mwinyi ameisisitiza timu hiyo ya Kitaalam kuhakikisha inamfikia kila mwanchi kote nchini ili kutoa maoni bila kujali tofauti za dini, siasa, jinsia, makundi maalum au eneo mtu analotoka kwani Rasimu hiyo ni ya Watanzania wote, hivyo alieleza ni lazima ibebe maono yao ya miaka 25 ijayo.

Kwa upandemwingine, Rais Dk. Mwinyi ameishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa kukusanya maoni ya wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na majadiliano na wadau.

Send this to a friend