Kijana wa miaka 20 ahukumiwa jela maisha kwa kumlawiti ndugu yake

0
5

Mashauri Ng’oga Shauri (20) mkazi wa kitongoji cha Mwankuba, kijiji cha Nyambiti, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mtoto wa baba yake mdogo (04) mkazi wa kijiji cha Nyambiti.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani Novemba 11, mwaka huu na kusomewa shitaka la kulawiti ambapo mashahidi wawili akiwemo mhanga pamoja na mzazi wake walitoa ushahidi baada ya kusomewa hoja za awali.

Baada ya kusikiliza mashahidi wanne wa Jamhuri, Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Kwimba, John Jagadi amejiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa dhidi ya mshtakiwa ni mzito na hivyo upande wa mashtaka umethibitisha shauri hilo pasi na kuacha shaka.

Mshtakiwa ameiomba mahakama hiyo imuachie huru kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, kitendo kilichopingwa na mwendesha mashtaka aliyeiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu kitendo hicho ni cha kinyama na cha ukatili uliopitiliza.

Hakimu Jagadi amesema licha ya mshtakiwa kuomba kupunguziwa adhabu, lakini kifungu kilichotajwa na mwendesha mashtaka hakina adhabu mbadala bali ni kumhukumu kifungo cha maisha.