Mahakama nchini Ufaransa imetangaza kumtia hatiani aliyekuwa mume wa Gisele Pelicot na washitakiwa wenzake 50 kwa kosa la kumlewesha hadi kupoteza fahamu kisha kuwaalika wanaume wengine kumbaka pasipo kujitambua.
Jopo la majaji watano katika mahakama ya jinai ya jiji la kusini mwa Ufaransa la Avignon limemhukumu Dominique Pelicot, mwenye umri wa miaka 72, ambaye alihusika kutekeleza mpango huo kwa washirika wenzake 50 ndani ya kipindi cha miaka 10.
Pelicot, ambaye alikiri kutenda makosa hayo wakati wa kesi iliyochukua takriban miezi mitatu, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, huku waendesha mashtaka wakitaka vifungo vya kati ya miaka minne na 18 kwa washitakiwa wengine.
Wanaume wengine 50 walioshtakiwa pamoja na Dominique Pelicot, ambao wengi wao walikana mashtaka, Mahakama ya Ufaransa iliwapata 46 kati yao na hatia ya ubakaji, wawili na hatia ya kujaribu kubaka na wawili na hatia ya unyanyasaji wa kingono.
Dominique Pelicot alijulikana kwa mara ya kwanza na polisi mnamo Septemba 2020, wakati mlinzi wa usalama wa duka alipomkamata akirekodi kwa siri chini ya sketi za wanawake.
Baadaye polisi walipopekua vifaa vyake vya kielektroniki, walikuta maktaba ya zaidi ya picha na video 20,000 za nyumbani zikionesha miaka ya unyanyasaji aliomfanyia mke wake, zikiwa zimehifadhiwa kwenye diski za kompyuta na kupangwa kwenye folda zenye majina.