Watu tisa wajeruhiwa kwa moto Songwe, Polisi yamshikilia mmoja

0
39

Watu tisa wamejeruhiwa kwa moto walipokuwa wakijaribu kuokoa mali kwenye duka la kuhifadhi na kuuza vinywaji vya jumla na reja reja katika kijiji cha Ihowa, Kata ya Ruanda mkoani Songwe.

Jeshi La Polisi limesema chanzo cha moto huo ni kitendo cha mke wa mmiliki wa kibanda, Rose Samweli ambaye alikuwa akifanya shughuli za kuwahudumia wateja huku akiendelea kupika ndani ya kibanda hicho ambacho kilikuwa kimehifadhi mafuta ya petroli, na ndipo moto ulipolipuka na kuunguza vitu.

Taarifa ya polisi imesema baada ya moto huo, watu waliokuwa wakiangalia mpira karibu na eneo hilo walikuja kwa ajili ya kutoa msaada, na katika harakati za kuokoa vitu ndipo walipoungua kwa moto.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linamshikilia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Patrick Mwachimbona kwa mahojiano kuhusu tukio hilo, na pindi upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Daktari wa Hospitali ya Vwawa wilayani Mbozi, Dkt. John Mwanyingili amesema majeruhi waliolazwa ni nane, saba kati yao wakiwa wanaume na mmoja akiwa mwanamke, ambapo majeruhi saba watahamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Songwe kwa matibabu zaidi.

 

Send this to a friend