Jeshi la Polisi mkoani Singida limekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mtu mmoja kutiliwa shaka na wafanyakazi wa basi namba T 794 EHR mali ya kampuni ya Frester ambalo lilikuwa likitokea Kahama kwenda Dar es Salaam kwamba anasafirisha kichwa cha mtu (mtoto) baada ya begi lake kutoa harufu kali likiwa ndani ya gari.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema Desemba 19, 2024 saa 12:30 jioni katika maeneo ya Mlima Senkenke, Wilaya ya Iramba mkoani humo, askari waliokuwa doria walipata taarifa ya taharuki na kufikia eneo la tukio kisha kumkamata mtuhumiwa anayejulikana kama Juma Lugendo (30) na kumpeleka kituo cha Polisi Misigiri kwa ajili ya upekuzi.
“Baada ya upekuzi, mtuhumiwa alikutwa na vifaa vya uganga wa kienyeji pamoja na dawa za kienyeji zilizochanganywa na utumbo mbichi wa samaki uliopelekea kutoa harufu kali ndani ya basi na sio kichwa cha mtu kama taarifa inavyosambaa kwenye mitandao ya kijamii,” imesema.
Jeshi la Polisi limesema mtuhumiwa amekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki katika jamii.